August 11, 2025
•
2 min read
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, leo Agosti 11, 2025 amefungua rasmi Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Polisi unaofanyika Shule ya Polisi Tanzania – Moshi, mkoani Kilimanjaro. Mkutano huo unaongozwa na Kauli mbiu isemayo “Amani, utulivu na usalama kabla, wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu 2025 ni jukumu letu sote” Akizungumza kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais ametoa pongezi kwa Jeshi la Polisi kwa kazi nzuri ya kulinda usalama wa wananchi na mali zao unaoendelea kufanywa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama. Alisema kuwa, amani na utulivu vinavyoendelea kushuhudiwa nchini ni matokeo ya juhudi kubwa zinazofanywa na vyombo hivyo, na kwamba maendeleo ya taifa hayawezi kupatikana pasipo msingi wa usalama. Pia, alisifu Kauli Mbiu ya mkutano huo isemayo: “Amani, Utulivu na Usalama Kabla, Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu 2025 ni Jukumu Letu Sote”, akisema inaendana na dhamira ya Serikali kuhakikisha uchaguzi wa amani na utulivu. Aidha, Mhe. Mpango alitumia jukwaa hilo kuwataka wananchi kujiepusha na vitendo vya uchochezi na uvunjifu wa amani, hasa katika kipindi hiki ambapo nchi imeanza mchakato wa uchaguzi kwa uteuzi wa wagombea. Alisisitiza kuwa madhara ya vurugu za kisiasa ni makubwa na yanagusa maisha ya kila mwananchi hivyo ni vyema kusimamia sheria. Vilevile alitoa pongezi kwa maandalizi ya Jeshi la Polisi kuelekea uchaguzi, ikiwemo kushirikiana na vyombo vingine, wadau wa uchaguzi na utekelezaji wa maelekezo ya Serikali katika kuhakikisha mazingira ya Uchaguzi yanabaki kuwa salama na tulivu.