Commandant wa Shule ya Polisi Tanzania – Moshi, SACP Ramadhan A. Mungi, amewataka wanafunzi wa Elimu ya Juu IAA–TPS Moshi kutumia elimu wanayoipata chuoni hapa ili kukabiliana na changamoto zinazoletwa na maendeleo ya teknolojia, hususan katika usalama wa mtandao na mifumo ya kidijitali.
Akizungumza katika Mdahalo wa Wanafunzi wa Elimu ya Juu uliofanyika chuoni hapo, Afande SACP Mungi alisisitiza kuwa maarifa, ubunifu na matumizi sahihi ya teknolojia ni nyenzo muhimu katika kuimarisha usalama wa taifa.
Mdahalo huo ulijadili mada muhimu zikiwemo Akili Bandia (AI) na athari zake kwa usalama, usalama wa mtandao, mabadiliko ya tabia ya nchi, usalama wa mipaka, ushirikiano wa kikanda, uhalifu unaovuka mipaka ya mataifa, pamoja na ujenzi wa taasisi imara za usalama kwa ajili ya kukabiliana na changamoto za sasa na zijazo.
Dawati la habari TPS-Moshi.